Katibu wa
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anapenda kuwataarifu
waombaji kazi waliofanya usaili wa mchujo kwa nafasi mbalimbali za
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa matokeo ya usaili huo yanatarajiwa kutolewa katika kipindi kisichozidi siku kumi (10) kuanzia siku ya tangazo hili.
Amesema kuwa
kutokana na muitikio mkubwa wa waombaji kazi waliojitokeza kwenye usaili
huo, kwa sasa zoezi linaloendelea ni kusahihisha mitihani hiyo ambayo
inatarajiwa kukamilika ndani ya muda huo. Ratiba kamili ya usaili wa ana
kwa ana (oral Interview) kwa kila kada itatolewa pamoja na majina ya
waliofaulu usaili wa mchujo.
Aidha,
amesisitiza waombaji kazi wote waliofanya usaili huo kuendelea kujiandaa
kwa ajili ya usaili unaofuata kwa wale watakaochaguliwa, ili kujiweka
katika nafasi ya kufanya vizuri kutokana na ujuzi na weledi walionao
katika taaluma zao na hatimae kuwa miongoni mwa watakaofanikiwa
kuajiriwa katika Utumishi wa Umma kupitia mamlaka hiyo.
Amewataka
wasailiwa watakaoitwa kwenye usaili wa mahojiano watatakiwa kuja na
vyeti vyao halisi kuanzia cheti cha kuzaliwa, cheti cha kidato cha nne,
kidato cha sita, Astashahada, Stashahada ya juu, Shahada na kuendelea
kulingana na kiwango cha elimu waliyonayo. Aidha kwa wale waliosoma nje
ya Nchi wafike na cheti cha uhakiki toka Mamlaka zenye dhamana ambazo ni
TCU, NACTE na NECTA.
Sambamba na hayo,
anawakumbusha wasailiwa hao kuendelea kutunza namba zao za usaili kwa
kuwa matokeo yote yatatolewa kupitia namba walizopewa wakati wa usaili.
Usaili huo wa
mchujo ulifanyika kwa muda wa siku tatu katika kanda kumi ambazo ni
Zanzibar, Mbeya, Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro, Mtwara, Tabora,
Iringa na Dar es Salaam kulikokuwa na vituo viwili vya usaili ambavyo ni
Chuo cha Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) na Chuo cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere, Kigamboni.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma tarehe 6 Septemba, 2017.
TANGAZO KWA WAOMBAJI KAZI WALIOFANYA USAILI WA NAFASI ZA TRA.
Reviewed by ISSAH JUMA
on
Tuesday, September 12, 2017
Rating:
No comments: